(ABNA24.com) Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameyasema hayo katika mazungumzo aliyofanya kwa njia ya simu na Amir wa Qatar Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani.
Rais Rouhani amesema, mashinikizo na vikwazo vya kidhalimu vya Marekani dhidi ya Iran ni ukiukaji wa kanuni za kimataifa na akasisitiza kuwa, viongozi wa Marekani wanakanyaga misingi ya kiutu kwa kuzuia Iran isipatiwe mkopo na Shirika la Kimataifa la Fedha (IMF).
Katika mazungumzo hayo ya simu, Dakta Rouhani ameashiria pia mipango na hatua zilizochukuliwa hapa nchini kwa ajili ya kupambana na maambukizo ya maradhi ya corona ya COVID-19, matibabu wanayopatiwa wanaougua maradhi hayo na sera zinazoratibiwa kwa ajili ya kutekeleza shughuli za kiuchumi, kiidara na za masomo; na akaeleza kwamba: Tehran iko tayari kuzipatia nchi zote na hasa Qatar, ambayo ni nchi ndugu na rafiki, tajiriba na uzoefu wake.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameeleza masikitiko yake pia kutokana na hujuma na mashambulio yanayoendelea kufanywa na muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia dhidi ya Yemen na kuendelezwa mauaji na uharibifu ndani ya nchi hiyo; na akabainisha kuwa: Kudhaminiwa amani na uthabiti endelevu hakuwezekani kwa njia yoyote ile zaidi ya ushirikiano na urafiki baina ya nchi za eneo.
Kwa upande wake, Amir wa Qatar Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani amesema, vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran ni vya kidhalimu na akaongeza kuwa: Leo hii dunia iko katika hali na mazingira maalumu; na Marekani inapaswa kuondoa vikwazo vyake na nchi zote pia zinapaswa kuchukua hatua kulingana na mazingira mapya yaliyopo.
Katika mazungumzo mengine aliyofanya kwa njia ya simu na Rais Yoweri Museveni wa Uganda, Rais Rouhani amesema: Inasikitisha kuona kwamba, licha ya mazingira magumu yaliyopo kutokana na maambukizo ya virusi vya corona, vikwazo vya kidhalimu na vya kinyume cha sheria vya Marekani dhidi ya wananchi wa Iran vingali vinaendelezwa.
Rais Yoweri Museveni wa Uganda, naye pia ameeleza masikitiko yake kutokana na hatua zilizo kinyume cha sheria zinazochukuliwa na Marekani dhidi ya Iran na akasema: Katika mazingira haya magumu, inapasa uhusiano wa kiutu upewe kipaumbele pamoja na kushajiisha kuishi kwa amani na masikilizano.
...............
340